Kwa mujibu wa Idara ya tarjama ya Shirika la Habari la Hawza, Hujjatul Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, Mkuu wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia nchini Pakistan, ametoa taarifa yake huku akisisitiza umuhimu wa umoja na udugu miongoni mwa Umma wa Kiislamu. Katika taarifa hiyo, ametoa wito wa kuepuka mivutano inayotokana na tofauti na kuzitaka nchi za Kiislamu kufanya juhudi za pamoja kwa ajili ya kupunguza mivutano ya kikanda na kufanikisha amani ya kudumu.
Katika kuendeleza msimamo wake, ameeleza wasiwasi mkubwa kuhusu kuongezeka mivutano na kuenea kwa hali ya kivita katika eneo hilo. Amesisitiza haja ya kuimarisha umoja wa Ulimwengu wa Kiislamu, kutumia fursa na uwezo uliopo katika diplomasia, na kushirikiana kwa pamoja miongoni mwa nchi za Kiislamu ili kumaliza migogoro ya kikanda.
Rais huyo wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia nchini Pakistan, akizungumzia uhusiano wa kiitikadi na udugu uliopo baina ya Waislamu, amesema: “Umma wa Kiislamu ni kama mwili mmoja, na wafuasi wa Mtukufu Muhammad Mustafa (s.a.w.w.), ambaye ni mwisho wa Mitume wa Mwenyezi Mungu, ni ndugu kwa wao kwa wao. Kwa hiyo, kukomesha hali hii ya sasa ya mgogoro na kuimarisha nafasi ya Umma wa Kiislamu ni wajibu wa pamoja unaozikabili nchi za Kiislamu na watu wenye dhamana na wajibu.”
Aidha, amesisitiza kwamba; Pakistan inapaswa kurejea tena katika kutekeleza jukumu hai na lenye kujenga, kwa kuchukua hatua katika njia ya kutatua tofauti, kupunguza mivutano na kuimarisha amani ya kudumu katika eneo hilo.
Hujjatul Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, akizungumzia maendeleo ya kikanda na misimamo ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Mujtaba Khamenei, pamoja na Sheikh wa Al-Azhar nchini Misri, Dkt. Ahmad al-Tayyib, ameeleza kuwa; mipango na mapendekezo yaliyotolewa na viongozi hao kuhusu amani, upatanishi na maridhiano ni yenye kuleta matumaini na yenye kujenga.
Amesema misimamo hiyo inaweza kusaidia kuimarisha utulivu wa kikanda, kupunguza mivutano, kukabiliana na changamoto za kiuchumi na kuweka mazingira yanayofaa kwa maendeleo na ushirikiano baina ya nchi za eneo hilo. Hata hivyo, amesisitiza kuwa kufikiwa malengo hayo kunahitaji maamuzi madhubuti pamoja na kuchukuliwa hatua za vitendo na za haraka.
Akizungumzia mapendekezo ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kuhusu upatanishi, pamoja na msimamo wa Sheikh wa Al-Azhar wa Misri unaounga mkono kuundwa mara moja kamati ya upatanishi na maridhiano, amesisitiza umuhimu wa kutumia fursa hizo.
Ameeleza kuwa kuundwa kamati ya aina hiyo, itakayojumuisha watu wenye ikhlasi, wenye mtazamo wa mbali, wenye busara na wanaopenda amani, kunaweza kuweka mazingira ya mazungumzo baina ya pande zinazohusika katika mzozo. Aidha, hatua hiyo inaweza kuwa mchango muhimu katika kupunguza tofauti na kufikia suluhisho za amani.
Mkuu huyo wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia nchini Pakistan, akirejelea ujumbe wa milele wa Qur’ani Tukufu kuhusu ulazima wa kushikamana na kamba ya Mwenyezi Mungu na kujiepusha na mifarakano, amesisitiza umuhimu wa kulinda umoja na mshikamano miongoni mwa Waislamu.
Amesema kuwa: Umma wa Kiislamu unapaswa kuweka kando tofauti zake na kujiepusha na kuchochea migogoro, ili kuweka mazingira ya kuimarika kwa udugu, maelewano na kuheshimiana. Ameongeza kuwa kupata heshima, maendeleo na nguvu kwa Ulimwengu wa Kiislamu kunategemea kuimarishwa kwa umoja miongoni mwa Waislamu na ushirikiano wa dhati baina ya nchi za Kiislamu.
Ameongeza kuwa katika mazingira haya nyeti, nchi za Kiislamu zinahitaji zaidi kuliko wakati mwingine wowote kuimarisha mshikamano, mazungumzo na kupitisha misimamo yenye uwajibikaji. Kwa kufanya hivyo, zitaweza kuvuka tofauti zilizopo na kuchukua msimamo wa pamoja katika kukabiliana na changamoto zinazozikabili kwa pamoja.
Hujjatul Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, akisisitiza ulazima wa Pakistan kuwa miongoni mwa nchi za kwanza kuchukua hatua katika juhudi za kuleta amani, amesema: “Pakistan, ikiwa ni nchi muhimu katika Ulimwengu wa Kiislamu na yenye uwezo wa kumiliki silaha za nyuklia, ina uwezo wa kutekeleza jukumu lenye athari katika kupunguza mivutano, kurahisisha mazungumzo na kuimarisha utulivu wa kikanda.”
Akizungumzia uwezo wa kidiplomasia wa Pakistan na uwezekano wa kupata imani ya pande mbalimbali, amebainisha kuwa nchi hiyo inapaswa kuongeza juhudi zake za kidiplomasia kwa kuchukua msimamo hai na wenye uwajibikaji, juhudi hizo zinapaswa kulenga kuleta karibu mitazamo ya pande zinazohusika, kuweka mazingira ya mazungumzo na kufikia suluhisho zinazokubaliwa na pande zote.
Rais huyo wa Baraza la Wanazuoni wa Kishia nchini Pakistan, akikumbusha nafasi ambayo nchi hiyo imewahi kutekeleza katika diplomasia ya kikanda hapo awali, amesisitiza umuhimu wa kufufua tena mkabala huo wenye kujenga. Aidha, ametoa wito kwa Pakistan kutekeleza wajibu mkubwa zaidi katika juhudi za upatanishi na kuleta amani.
Ameongeza kuwa matokeo ya juhudi hizo hayatakuwa tu katika kupunguza mapigano na kuimarisha usalama wa kikanda, bali pia yanaweza kupunguza athari hasi za mivutano kwa uchumi wa nchi za eneo hilo, kupanua wigo wa ushirikiano wa pande zote na kufungua fursa mpya za maendeleo na ustawi.
Hujjatul Islam wal-Muslimin Sayyid Sajid Ali Naqvi, akisisitiza umuhimu wa kutumia uwezo na fursa zote zilizopo ili kudhibiti mgogoro wa sasa, ametoa wito wa kujiepusha na kauli zinazoongeza mivutano na misimamo inayochochea uhasama.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuwa macho dhidi ya njama za maadui na kuzuia kuongezeka tofauti. Amebainisha kuwa katika mazingira haya nyeti, badala ya kuchochea migogoro, ni muhimu kuelekeza nguvu katika kuimarisha umoja, maelewano ya pande zote, mazungumzo na suluhisho za kidiplomasia.
Amemalizia kwa kubainisha kuwa; ushirikiano baina ya nchi za Kiislamu, kuimarishwa kuaminiana na kuungwa mkono mipango ya kuleta amani kunaweza kuweka mazingira ya kuepuka migogoro iliyopo na kurahisisha njia ya kufikia amani na utulivu wa kudumu katika eneo hilo.
Maoni yako